Monday, February 3, 2014

Ijue kwaya ya vijana kijitonyama

KWAYA YA VIJANA KIJITONYAMA

MFUMO WA UIMBAJI KATIKA KWAYA YETU

Kama yalivyoandaliwa na:
Mwalimu wa kwaya; Gadiel Ketto.
October 16, 2002
Yafuatayo ni mapendekezo ya taratibu za uimbaji katika kwaya ya vijana. Msukumo wa
mapendekezo haya ni kuweka mfumo mzuri na madhubuti usio badilikabadilika kulingana na mabadiliko yoyote yayoweza kutokea katika kwaya. Mabadiliko yaweza kusababiswa na kubadilika kwa waimbaji, waalimu, au viongozi. Pia misukumo toka nje ya kwaya yaweza pia kuleta mabadiliko. Hivyo ili tuweze kuwa na mfumo imara wa uimbaji, tunapendekeza yafuatayo:-

1. AINA YA UIMBAJI
Aina ya uimbaji ni ile inayombariki Mungu na wanadamu. Lakini wanadamu huwa wana
vionjo vingi na vinavyotofautiana. Hivyo ili tuweze kumgusa kila mtu yafaa sisi kama
waimbaji au wasanii tuweze kuangalia kuwa hadhira inataka nini kwa ujumala bila kuangalia na kuridhisha sehemu tu ya kundi la watu. Faida yake ni kuwa ujumbe wetu katika nyimbo utaweza kuyagusa makundi yote katika jamii na kufanikisha malengo yetu. Kwa hiyo basi tuwe na uimbaji wa aina mbalimbali kama vile pambio, nyimbo za haraka haraka, nyimbo za taratibu na nyimbo za kawaida zilizozoeleka katika muziki wa kanisani.

2. NYIMBO
Kama kwaya tunapaswa kujifunza na kuimba nyimbo mbalimbali. Ni vyema nyimbo zetu
zikawa katika makundi yafuatayo:-
a).Nyimbo za zamani (classic music)
Hizi ni nyimbo zilizoandikwa zamani ambazo zina "melody" nzuri na ujumbe mzuri.
Hizi zifundishwe na.kuimbwa katika kwaya yetu.
b).Nyimbo za kutunga / kuandika wenyewe (contemporary music).
Nyimbo hizi ni nzuri zaidi, zinachochea ubunifu na vipaji tulivyonavyo. Ni vizuri tukaandika na kuimba nyimbo kulingana na jamii ya sasa na kwa faida ya vizazi vijavyo. Tukumbuke kuwa hata nyimbo za zamani tunazoimba leo ziliandikwa na watu kwa msaada wa Roho Mtakatifu. Kama babu zetu wasingeandika tusingekuwa na nyimbo nzuri za kuimba kama tunavyofahamu. Kwa hiyo tujue kuwa kama hatutaandka nyimbo leo, watoto wetu hawatakuwa na kitu cha kujivunia ambacho tumewarithisha kwa ajili ya Bwana. Pia tukwepe kuimba nyimbo za watu wengine, walioandika wenyewe na kuimbwa na watu wengine kwa kuzingatia sheria ya haki-miliki tukijua kuwa hata tukiimba hatuwezi kuzirekodi.

3. MUZIKI / ALA (ACCOMPANIMENT)
Ni vizuri kumwimbia Mungu kwa kutumia vyombo mbalimbali ambavyo vinasaidia
kuusindikiza ujumbe. Vyombo hivyo ni kama gitaa, keyboard, tarumbeta, ngoma, nk.
Inafaa kuwa na utaratibu mzuri wa kuvitumia bila kuleta fujo na kelele katika uimbaji. Hili tu litawezekana endapo tutatafuta na kuwaandaa wanamuziki wetu katika kwaya hii.

4. UFUNDISHAJI WA NYIMBO
Kwaya nzuri ni ile yenye waalimu wengi angalau watano wenye vipaji na utaalamu katika fani ya muziki. Hawa lazima wawe na sauti moja ili kifanya kwaya iwe moja uimbaji mmoja na usiobadilika. Kiburi na kujikweza iwe mwiko kwa walimu wa kwaya hii. Pia kuwe na utaratibu mzuri wa kufundisha nyimbo kwa kupeana nafasi na kushirikiana katika kuboresha. Kwa upande huu pia ni vyema wale wenye vipaji wakatiwa moyo ili kusomea fani ya muziki.

5. UBORESHAJI WA UIMBAJI
Kama waswahili wasemavyo ukiamua kumla nguruwe chagua aliyenona, vivyohivyo na
sisi kama tumenamua kuimba ni vyema tukaimba vizuri. Hivyo ni vizuri tukazingatia mazoezi ya mara kwa mara ya uimbaji na kuhakikisha kuwa kila mwanakwaya anashiriki. Mazoezi haya yafanyike kila siku za mazoezi, kuandaa kambi, na hata kufanya mikesha maaalumu ya mazoezi ya uimbaji.

No comments:

Post a Comment